Seneta Wambua amrai Malombe kutomtatiza Ngilu.

0
2721
Kitui Senator, Hon Enoch Kiio Wambua

Seneta wa Kitui Enoch Wambua hii leo ameinglia kati kesi iliyo mahakamani kupinga ushindi wa Ngilu.Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani na aliyekuwa gavana Julius Malombe.Seneta Enoch Wambua amemrai Malombe kuiondoa kesi hiyo mahakamani.

Akiwahutubia watu katika kituo kidogo cha kibiashara cha Katulani hapo jana,Wambua alitetea vikali ushindi wa Ngilu.Seneta huyo alisema ushindi wa Ngilu ulikuwa wa njia halali.Wambua alikuwa amejumuika pamoja na wakazi wa Kitui kushiriki siku ya kuadhimisha ugonjwa hatari wa ukimwi duniani.Wambua alisema kwamba hatua ya Malombe ya kumshtaki Ngilu inaathiri pakubwa utendakazi wake kama gavana.

Aliongeza kwamba ngilu hawezi kuwahudumia kikamilifu wakazi wa kitui kesi hiyo ikiwa mahakamani.Hii ni kwa sababu wakati mwingine atahitajika kufika mahakamani kujitetea.Seneta aliitaja kesi hii kuchangiwa na misimamo kinzani ya kisiasa.Wambua alimtaja Ngilu kuwa katika njia panda kutokana na kesi hiyo inayotatiza pakubwa utendakazi wake na kuizuia sera za maendeleo na mipango aliyowaahidi watu wa kitui wakati wa kuomba kura.

Pia Seneta Wambua aliwarai wazee kutoka jimbo la kitui kumtembelea nyumbani kwake na kufanya majadiliano naye ili aweze kubadilisha msimamo wake mkali.Hatua hii inalenga kumshawishi Malombe kuiondoa kesi hiyo mahakamani.Aliongeza kwamba watu wa Kitui hawatatazama kuona utendakazi wa Ngilu ukilemazwa na wachache walio na nia ya kujinufaisha wenyewe.Malombe alibwagwa chini na Mama Ngilu katika uchaguzi wa Agosti nane mwaka huu.

Malombe alienda mahamani baada ya kupoteza katika uchaguzi mkuu wa 8/8/2017.Baada ya matokeo ya mwisho kutangazwa,Malombe alikimbia mahakamani kumpinga Ngilu. Gavana Ngilu alishinda uchaguzi huo kwa asilimia kubwa zaidi.Mshindani wake wa karibu sana alikuwa aliyekuwa Seneta David Musila. Malombe aliibuka wa tatu katika uchaguzi huo.

Malombe alisema uchaguzi huo ulikuwa na dosari nyingi hivyo basi hangeweza kukubaliana na matokeo yake.Malombe analenga mahakama kutupilia mbali ushindi wa Ngilu na kuamrisha kuandaliwa tena kwa uchaguzi mpya.Kesi hiyo inatarajiwa kusikizwa Alhamisi ,Desemba 7, 2017.Malombe amewasilisha mashahidi 15 kutoa ushahidi wao mbele ya mahakama.

Facebook Comments