Kitui: Mama Kaunti kuomba Wakaazi kujitokeza kwa wingi kupimwa ugonjwa wa Saratani.

0
1646
Mwakilishi wa akina mama kutoka gatuzi la Kitui Mheshimiwa Irene Kasalu

Mwakilishi wa akina mama kutoka gatuzi la Kitui Mheshimiwa Irene Kasalu aliwarai watu kujitokeza kwa wingi wapate kupimwa ugonjwa wa saratani.Mwakilishi huyo wa Wanawake alionyesha kuhuzunika kwake kutokana na idadi kubwa ya Wakenya wanaopoteza maisha yao kutokana na kuugua ugonjwa huo.

Kulingana na takwimu za hospitali kuu za kitaifa hapa Kenya,ni bayana kwamba ugonjwa huo umekuwa miongoni mwa magonjwa yanayoangamiza Wakenya wengi na hata pia barani Afrika.

Mbunge huyo aliyasema hayo hapo jana Jumamosi 27Januari,2018 alipohudhuria mazishi katika sehemu tofauti zilizo katika Wadi ya Mbitini eneo bunge la Kitui Rural.

Kwa upande wa wanawake saratani ya matiti na ya mfuko wa uzazi imekuwa sugu huku ikiangamiza idadi kubwa ya wanawake.Wanaume nao wamekuwa wakivamiwa na kansa ya kibofu.Jinamizi hili la ugonjwa limesababisha watoto wadogo kwa wakubwa kuachwa mayatima na pia baadhi yao kufariki wakiwa na umri mpevu kutokana na athari za kansa.

Kasalu hakusahau kuzungumzia suala la ubakaji kwa wasichana wenye umri mdogo na wanaume.Aliwaonya kina mama kutonyamazia visa kama hivyo vinapotendeka na badala yake kuwashauri wawe wakipiga ripoti kwa Machifu na Manaibu wao ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahalifu wanaoptatikana na hatia.

Hatimaye, Mbunge huyo alisema kwamba afisi yake itatenga kiasi fulani cha pesa kufadhili elimu kwa wanawake ili kuwafunza njia mwafaka wanazofaa kuchukua baada ya visa kama hivyo kufanyika.

Facebook Comments