Kitui: Mama kumtupa mwanawe katika shimo la choo.

0
1528

Kitoto kutolewa katika shimo la choo Jumatatu 30 Januari, 2018 Kitui.

Maafisa wa polisi katika eneo bunge la Kitui Magharibi kuendeleza msako wa kumsaka mwanamke anayedaiwa kujifungua na kumtupa malaika katika shimo la choo kwa sababu ambazo hazijulikani.

Kitoto hicho kilipatikana kimetupwa ndani ya choo cha ajuza mmoja mwenye umri wa zaidi ya miaka 65. Mtoto huyo mchanga alitolewa kutoka katika choo alikotupwa kutokana na ushirikiano wa karibu na wakaazi wa kijiji cha Kakeani katika Wadi ya Mutonguni eneo bunge la Kitui Magharibi.

Akithimbitishwa kisa hicho ,Chifu wa Kata hiyo ya Kakeani Bwana Patrick Musili Ndoo alisema ya kwamba iliwakazimu wakaazi wa eneo hilo kukibomoa choo hicho ili kukitoa kitoto hicho katika shimo hilo la choo.Ushirikiano wa karibu baina ya wanakijiji ulisababisha juhudi zao kuzaa matunda na kumuokoa malaika huyo angali hai.

Baada ya kuokolewa kutoka lindi hilo la mauti,kitoto hicho kilipelekwa katika zahanati ya Kakeani kupata huduma ya kwanza .Hapo baadaye kitoto hicho kilipata kuhamishiwa katika hospitali kuu ya serikali ya jimbo la Kitui ili kupata matibabu zaidi.Kwa sasa kitoto hicho kiko mikononi mwa madaktari.

Chifu huyo aliongeza kwamba msako mkali umeanzishwa na maafisa wa polisi ili kumtia mikononi mama au msichana aliyemzaa mtoto huyo na kuamua kumtupa katika shimo la choo.Aliwaomba wanakijiji kushirikiana kwa karibu na maafisa wa polisi ili kumkamata aliyetekeleza kisa hicho.

Hata hivyo,Chifu Musili alisema kwamba ni jambo la kuhuzunisha kuona visa kama hivyo katika eneo la Kakeani.Aliwaonya wote walio na tabia kama hizo kuzikomesha mara moja.Aidha,aliongeza kwamba wote walio na nia mbaya kama hizo hawana budi kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Facebook Comments