Serikali Kuendesha Msako wa Kuwasaka Wahalifu Makueni.

0
1480

Kamishna Msaidizi wa Tarafa ya Kilala jimbo la Makueni Bwana Bernard Nicholas usiku wa kuamkia Jumapili ya leo Februari 11,2018 ameongoza msako wa kuwasaka wote wanaoendeshesha biashara haramu za kuuza pombe iliyopigwa marufuku na serikali pamoja na walanguzi wa bangi.

Katika msako huo ulioanzishwa jana Jumamosi usiku mwendo wa 11:30 na kukamilika takriban saa 3:00 asubuhi ya leo viringisha 73 za bangi zilipatikana. Pia, zaidi ya kilo moja ya bangi ilipatikana pamoja na pombe haramu yenye kiasi kisichopungua lita 900.Lita 580 zilimwagwa baada ya kupatikana Kata-Ndogo ya Iuani kwa mgema maarufu Sila na zingine 300 kusafirishwa na maafisa hao wa utawala hadi kituo cha polisi kwa minajili ya kutumika kama ushahidi mahakamani dhidi ya wagemaji hao.

Akizungumza na Wanahabari baada ya kuendesha zoezi hilo,Bwana Bernard alisema kwamba wagema waliopatikana na pombe hiyo pamoja na mlanguzi wa bangi watafikishwa kizimbani punde watakapopatikana. Mlanguzi wa bangi pamoja na wenzao wa pombe hiyo almaarufu “Kaluvu” walitorokea usalama wao wasipate kutiwa nguvuni na maafisa hao.

Hata hivyo,Kamishna huyo aliongeza kwamba maafisa wa polisi bado wanaendeleza juhudi za kuwasaka ili kuwatia wahalifu hao.

Kamishna pia aliwaonya wagema wote wanaojihusisha katika zoezi la kutua pombe hiyo haramu kwamba sheria haitawasaza kamwe kutokana na matendo yao yanayokiuka sheria za nchi. Aliongeza kwamba wataendeleza misako katika eneo hilo ili kuhakikisha kwamba wote wanaoenda kinyume na sheria za nchi wamekabiliwa na mkono wa serikali.

Usemi wa Kamishna Bernard uliungwa mkono na Kaimu Msaidizi katika Jimbo- Ndogo la Makueni Bi. Florence Obuga.Naibu Kamishna huyo aliwarai wote wanaoendeleza shughuli za kutua na kuuza pombe haramu kukoma kabisa kabla ya mkono mrefu wa serikali kuwanasa.

Bi. Florence aliwashauri wagema hao kutafuta njia m-badala ya kuendesha maisha na kujiepusha na matendo yoyote ya kihalifu yanayoweza kusababisha wao kutiwa mbaroni na hata kufungwa korokoroni kuhudumia uhalifu wao.

Hawa wawili kwa pamoja walitoa onyo kali kwa Naibu- Chifu wa Nthangu pamoja na Mzee wa kijiji cha Kitutu kwa vile wameruhusu visa vya utuaji pombe haramu katika eneo hilo.Pombe hiyo yasemekana kuwa husafirishwa hadi soko la Yiuani na kuuzwa kwa wakaazi rasmi wa hapo. Waliongeza kwamba karibuni hawa wawili watakamatwa iwapo visa vya ugemaji pombe hazitakoma katika sehemu zao.

Facebook Comments