Mheshimiwa Kaki Nyamai awatahadharisha wakaazi wa kitui kutovuka mito iliyofurika.

0
1858
Hin Rachel Kaki speaking at Ilamba Primary School, Kitui South

Ilikuwa ni furaha ghaya kwa familia kuungana na jamaa wao baada ya juhudi za kuwaokoa watu watano waliokuwa wamezuiliwa na maji katika vijiji vya Maluuma na Matikoni eneo bunge la Kitui Kusini kufua dafu kutokana na ushirikiano wa karibu kati ya wanakijiji na maafisa wa kupambana na majanga ya dharura jimbo la Kitui.

Watano hao ambapo wanne ni watoto wenye umri mdogo na mwanamke mmoja mwenye umri wa makamo walithibitishwa kuzuiliwa katika mazingira yaliyohatarisha usalama wa maisha yao siku ya Jumanne 24/04/2018 mwendo wa jioni baada ya kiwango cha maji katika mto Thua kuongezeka kufuatia mvua kubwa iliyonyesha jioni hiyo.

Baada ya kiwango cha maji kuzidi kuongezeka iliwalazimu watano hao kutafuta njia m-badala ya kuyaokoa maisha yao.Hatua waliyoichukua ilikuwa ni kukwea mti angalau kujihakikishia usalama wao.

Wakaazi wa maeneo hayo walilazimika kuchukua hatua za dharura ili kuwanusuru watano hao kutoka vileleni mwa miti waliyoikwea angalau kuyalinda maisha yao kutokana na jinamizi lililowakumba wasijue hatima yao wala la kufanya ili kujikomboa kutoka pale waliponaswa

Mbunge wa eneo hilo Mheshimiwa Rachael Kaki Nyamai aliwapongeza wakaazi wa vijiji hivyo kwa ushirikiano wao na maafisa wa kukabiliana na majanga ili kukomboa maisha ya watano hao.

Kufikia sasa mito mingi katika Jimbo-Ndogo za Mutomo na Ikutha katika eneo bunge la Kitui Kusini imethibitishwa kufurika na hata kuvunja kingo zake kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika sehemu nyingi katika jimbo hilo.

Aidha, Mbunge huyo anatahadhari watu wanaoishi karibu na kingo za mito ya Athi,Nzeeu,Thua na Tiva kutokaribia pale wala kuwatuma watoto wadogo mitoni msimu huu wa mvua ya vuli kwa sababu za ki-usalama wao.Anasisitiza kuwepo haja ya kulinda maisha ya kila mtu dhidi ya ajali za mitoni ambazo zimekua zikitokea mara kwa mara kwa kipindi cha miezi michache iliyopita katika sehemu tofauti nchini.

Wakaazi wa sehemu hiyo wanashauriwa kutokaribia mashamba yao yaliyo karibu na mito ili kujiepusha na hatari za kusombwa na maji .

Iwapo wanakijiji wangechelewa kuwanasua watano hao pale waliponaswa hali ingezidi kuwa mbaya zaidi kutokana na kuongezeka kwa maji jinsi mvua ilivyozidi.

Facebook Comments